Nafasi Ya Matangazo

February 13, 2017

 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Rebecca Kwandu akizungumza na wajumbe wa kikao cha mafunzo ya Maafisa Habari na TEHAMA kutoka katika Halmashauri na Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera na Simiyu wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Jijini Mwanza.  Kulia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo, Johnsen Bukwali.
 Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Mawasiliano ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta ya Umma, Desderi Wengaa akizungumza na wajumbe wa kikao cha mafunzo ya Maafisa Habari na TEHAMA kutoka katika Halmashauri na Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera na Simiyu wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo Jijini Mwanza.  Kulia ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo, Johnsen Bukwali
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza, Johnsen Bukwali katikati (walipokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina ya mafunzo elekezi kwa Maafisa Habari na TEHAMA kutoka katika Hallmashauri na Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Kagera na Mara mara baada ya kufungua mafunzo hayo leo Jijini Mwanza
****************
SERIKALI imewataka Maafisa Habari na Maafisa Tehama katika sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya nchini kuweka taarifa sahihi zenye kuzingatia muda na wakati ili kuongeza ufanisi wa kutangaza shughuli za Serikali kwa umma.

Hayo yamesemwa leo Jijini Mwanza na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Clodwig Mtweve, katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi, Johnsen Bukwali wakati wa mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa katika tovuti yaliyoandaliwa na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Umma (PS3) kwa Maafisa Habari na Tehama wa Halmashauri na Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera na Simiyu.

Kwa Mujibu wa Mtweve alisema uwekaji taarifa katika tovuti hizo zitasaidia kuimarisha shughuli za utawala na kuifanya Serikali kufahamika zaidi kwa wadau wake na hivyo kupunguza malalamiko ya mara kwa mara yanayotolewa na wananchi kuhusu huduma zake kwa umma.

“Ninyi ndio mmekuwa wachakataji wa taarifa za Serikali na kuhakikisha zinaufikia umma wa Watanzania zikiwa katika hali ya ubora kwa kutumia njia mbali mbali za mawasiliano kama vile mbao za matangazo na hata kwa njia ya mitandao” alisema Mtweve.

Kwa mujibu wa  Mtweve alisema kuwa lengo la Serikali ni kuongeza uwazi na wigo wa upatikanaji wa taarifa sahihi na zenye uhakika katika tovuti zake ili kuiepusha Serikali na habari za kuzusha na zisizo na maslahi kwa taifa.

Aidha Mtweve pia aliwataka Watendaji wa Serikali hao kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanatoa fursa kwao katika kujibu maswali mbalimbali ya wananchi yanayoulizwa kupitia mitandao ya kijamii na hivyo kuwawezesha kufahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kutekelezwa katika Mikoa na Halmashauri zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Mawasiliano katika Mradi wa (PS3), Desderi Wengaa alisema mradi huo unatelezwa katika Mikoa 13 Bara na Halmashauri 93 za Tanzania Bara, ambao katika awamu ya kwanza itahusisha washiriki kutoka mikoa ya kanda ya Ziwa pekee.

Aliitaja mikoa inayotekeleza mradi huo kuwa ni Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera, Rukwa, Mbeya, Iringa, Dodoma, Morogoro, Njombe, Mtwara, Kigoma na Lindi.

Wengaa alisema mradi wa PS3 umejikita katika maeneo makuu manne ya utawala bora, usimamizi wa rasilimali watu, rasilimali fedha pamoja na mfumo wa mawasiliano ndani ya Serikali.

“Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo Maafisa Habari na TEHAMA katika Mikoa na Halmashauri kuweka taarifa katika tovuti zao ambazo zitasaidia wananchi kufahamu kwa ukaribu zaidi shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika maeneo yao” alisema Wengaa.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Rebecca Kwandu alisema ili mafunzo hayo yalete tija iliyokusudiwa ni wajibu wa Maaafisa Habari na TEHAMA washirikiane kwa karibu zaidi ili kuhakikisha taarifa taarifa muhimu zilizopo katika maeneo yao ya kazi zinawafikia wananchi katika muda na wakati uliowekwa.
Posted by MROKI On Monday, February 13, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo