Nafasi Ya Matangazo

January 07, 2017

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nane wa Majaji Wanawake ulioandaliwa na Chama Cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) unaofanyika kila baada ya miaka miwili na mkutano wa mwaka huu ulikuwa na kauli mbiu isemayo Kuongoza njia kufikia hitajio la upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati.
 Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akihutubia wakati wa mkutano wa nane wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania uliofanyika kwenye ukumbi wa PSPF Golden Jubilee jijini Dar es Salaam.
 Mhe. Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar,Mhe. Othman Makungu,akitoa nasaha zake wakati wa uzinduzi wa mkutano wa nane wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
 Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania Jaji Imani Aboud akitoa salaam za ufunguzi wa mkutano wa nane wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
Sehemu ya waliohudhuria wakiwa makini katika kuchukua yale yaliosemwa na Mhe. Makamu wa Rais wakati wa uzinduzi wa mkutano wa nane wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA)
***************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaagiza Majaji na Mahakimu wanawake kote nchini kupambana ipasavyo katika kukabiliana vitendo vya rushwa,unyanyasaji kijinsia na rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi bila kubaguliwa katika jamii.

         Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam wakati anafungua Mkutano Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA).

         Makamu wa Rais pia ameonya kuhusu vitendo vya rushwa ya ngono inayofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka na kusema tabia hiyo ni mbaya na lazima ikomeshwa mara moja katika jamii.

         Amesema kuwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono huzuia na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za kiserikali ipasavyo ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa wanawake.

          Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekishukuru Chama cha Dunia cha Majaji Wanawake (IAWJ) kwa mchango na msaada wake kwa TAWJA katika programu ya miaka mitatu ya kupambana na matumizi mabaya ya madaraka na rushwa ya ngono.
         
       Makamu wa Rais pia ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria, Shirika la UN Women na wadau wengine wa TAWJA kwa kuunga mkono mapambano ya aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.
        
       Amesema elimu ya haki za Binadamu iliyotolewa na Chama hicho imeleta badiliko kwa wengi kwa njia ya mafunzo na machapisho na jitihada hivyo lazima ziongezwe ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini.
        Amesisitiza wanachama wa Chama cha TAWJA waendelee kutoa msaada katika kuwasaidia wanawake na watoto ambao wanakandamizwa kwa kunyimwa haki zao katika jamii ili waweze kupata haki zao nchini.

              Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mohamed Chande Othman amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa mkakati wa uimarishaji wa shughuli za mahakama nchini unaendelea vyema lengo likiwa ni kutenda haki kwa wananchi kote nchini bila ubaguzi.
            Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (TAWJA) “Kuongoza njia kufikia hitajio la upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati”.
Posted by MROKI On Saturday, January 07, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo