Nafasi Ya Matangazo

November 09, 2016

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa Dola za Marekani 33,000 (sawa na sh. milioni 71) kutoka kwa makampuni ya Kuwait ili ziwasaidie wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo (Jumatano, Novemba 9, 2016), Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Bw. Jasem Al-Najem amesema msaada huo ni mchango kutoka kwa  Mwenyekiti wa Umoja wa Makampuni ya Fouad Alghanim, Bw. Fouad Alghanim aishiye Kuwait.

Amesema watu kadhaa wameguswa na maafa yalitokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu na wameamua kuchangia ili kuisaidia juhudi za Serikali kukabiliana na hali hiyo ambayo haikutarajiwa.

“Tunatambua kuwa kazi ya kurejesha huduma kwa wananchi ni kubwa, na Serikali peke yake haiwezi kubeba mzigo wa kukarabati miundombinu na majengo ya ofisi na makazi ili kuurejesha mkoa huo katika hali yale ya kawaida,” amesema.

Akizungumza na Balozi Al-Najem ofisini kwake Bungeni, mjini Dodoma, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Tanzania imeguswa na moyo wa upendo kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Makampuni ya Fouad Alghanim na wenzake.

Akitoa shukrani kwa msaada huo, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha mchango huo unafikishwa Kagera kwa walengwa.

Tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka huu lilisababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa. Pia lilisababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi na 9,471 zikipata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
Posted by MROKI On Wednesday, November 09, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo