Nafasi Ya Matangazo

October 12, 2016



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akisikiliza taarifa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Martin Mkisi mara baada ya kutembelea ofisi hizo mkoani Kigoma.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali (Mstaafu), Emmanuel Maganga,    akikabidhi taarifa ya maendeleo ya miundombinu ya mkoa wake kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipomtembelea ofisini kwake.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kulia), akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa mkoani Kigoma, Bw. Peter Mlonganile wakati alipotembelea chuo hicho.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akikata moja ya nondo katika ujenzi wa Daraja la Muzye lililopo kwenye barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 50 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto), akitoka kukagua ujenzi wa daraja la Muzye lililopo kwenye barabara ya Kidahwe- Kasulu KM 50 wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo. Wa pili kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma.



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akikagua moja ya vifaa vinavyotumika kupima aina ya udongo unaotumika kujengea barabara katika maabara iliyopo kwenye kambi ya Mkandarasi anayejenga barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 50. Wa Pili Kulia ni Mhandisi wa Maabara kutoka kampuni China Railway 15th Group Eng. Raphael Ndimbo.



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya ya Kibondo,alipotembelea ofisi hizo mkoani Kigoma.
******************
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi  kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria madereva wote wa malori ya mchanga na kokoto  watakaobainika kutofuata sheria za ubebaji wa bidhaa hiyo na hivyo kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.



Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani  Kigoma  katika ziara yake ya kukagua barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa kilometa 50 ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla hivyo haita mvumilia mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombu hiyo kwa makusudi.

“Kuanzia sasa Serikali haitavumilia madereva wasiozingatia kanuni na sheria za usafirishaji wa mizigo katika barabara nchini, hivyo nawaagiza Mameneja wa TANROADS katika mikoa yote nchini kusimamia sheria ili kudhibiti miundombinu ya barabara, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ameliomba Jeshi la Polisi kushirikiana vema na makandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wanaiba vifaa vya makandarasi jambo linalochangia kukwamisha shughuli za ujenzi wa barabara.

Amewataka wananchi wa Wilaya ya Kasulu kutoa ushirikiano kwa mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara hiyo ili kuwezesha ujenzi huo kukamilika haraka.

Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma, amebainisha changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni wizi wa mafuta na vifaa vya ujenzi hali inayosababisha mradi kusuasua.

"Wananachi tambueni kuwa fedha hizi ni za kwenu mnapohujumu vifaa vya ujenzi ni dhahiri mnajicheleweshea maendeleo na kukwamisha fursa za kiuchumi katika wilaya yenu", amesema Eng. Choma.

Kwa upande wake Mhandisi Mkazi Mekbib Tesfaye anayesimamia mradi huo kutoka Kampuni ya DOCH Limited, amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24 ambapo kwa sasa kazi inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili na makalvati katika barabara hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea Chuo cha Mamlaka ya Hali ya Hewa Mkoani Kigoma na kuahidi uongozi kuwa atazishughulikia  haraka changamoto kadhaa zinazokikabili chuo hicho  ili kuweka mazingira rafiki  ya kujisomea kwa wanafunzi wanaosomea taalauma hiyo. 

“Nitahakikisha chuo hiki kinajengewa mabweni ya wanafunzi pamoja na kuongeza gari kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazofanyika hapa”, amefafanua Waziri Mbarawa.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Peter Mlonganile wakati  akisoma taaraifa ya chuo hicho kwa Waziri huyo amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto hizo  chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo  hayo kwa  viwango vinavyotakiwa  ikiwa ni pamoja na kuzitatua changamoto ndogo ndogo zinazo kikabili chuo hicho.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, katika mkoa wa Kigoma ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu hiyo na kuuwezesha mkoa kufanya biashara kirahisi na mikoa mingine ya Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.

Posted by MROKI On Wednesday, October 12, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo