Nafasi Ya Matangazo

August 21, 2016

 Mkurugenzi Mkuu wa TBL Group akiongea na  waandishi wa habari
 Waandishi wa habari wakipatiwa maelezo wakati walipotembelea kiwanda cha TBL  cha Mwanza
 Waandishi wa habari wakipatiwa maelezo wakati walipotembelea kiwanda cha TBL  cha Mwanza
Mkurugenzi Mkuu wa  TBL Group,Roberto Jarrin,amesema kuwa mtazamo wa kuifanya Tanzania nchi ya viwanda unawezekana kutekelezeka kwa vitendo na kuongeza kuwa kampuni yake itaendeleza mkakati wake wa kuchangia kuleta mabadiliko nchini Tanzania kwa kuchangia kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta mbalimbali zinazohusiana na kampuni hiyo.

Akitoa mwelekeo wa utendaji wa kampuni yake kwa waandishi wa habari jijini Mwanza mwishoni mwa wiki alisema “Mbali na kampuni  yetu kuchangia pato la serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni 384/- kwa njia ya kodi imekuwa ikiziwezesha sekta nyinginezo inazoshirikiana nazo kibiashara kuanzia kwa wakulima wa nafaka mbalimbali hadi  kwa watumiaji wa mwisho wa bidhaa zetu.”BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

Alisema kampuni itawekeza zaidi kiasi cha shilingi bilioni 27/- katika kuwezesha maelfu ya wakulima wa mazao ya Shahiri,mtama na mahindi kuongeza mavuno kutokana na kulima kwa njia za kisasa-Wakulima watapatiwa utaalamu wa kilimo,mbegu bora na udhamini kupata mikopo ya kuendesha kiilimo cha kisasa kutoka kwenye mabenki inaoshirikiana nayo ambayo ni CRDB,NMB na Bank Of Africa (BOA).

Jarrin alisema kampuni pia imechochea kukua kwa  sekta ya usafirishaji nchini na kunufaisha jamii na kuchangia pato la serikali ambapo imetumia kiasi cha shilingi bilioni 150/-katika usafirishaji wa  malighafi mbalimbali kutoka zinapozalishwa hadi kwenye viwanda vake pia wamekuwa wanasafirisha bidhaa zinazozalishwa na kampuni kutoka viwandani hadi kwa watumiaji wa bidhaa hizo waliosambaa nchini kote.Mwaka wa fedha wa kampuni ya TBL Group umeanza tarehe 1 Aprili mwaka huu na utaisha tarehe 30 ya mwezi Machi mwaka ujao wa 2017.

Alisema kampuni itaendelea kutekeleza mpango wa kilimo shirikishi na wakulima wanaozalisha mazao ya Shahiri,Mtama , mahindi na Zabibu nchini ambayo inayatumia kama malighafi kwa ajili ya viwanda vyake na itahakikisha wanapata mazao ya ziada kwa ajili ya kuboresha maisha yao  na watasaidiwa kuunganishwa na masoko mazuri ya kuuza mazao ya ziada kutoka taasisi zinazonunua mazao hususani nafaka kwa ajili ya kusaidia jamii zenye upungufu wa chakula kama vile Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa.

Kilimo cha Shahiri kinawawezesha wakulima  zaidi ya 3,000 wanaoishi vijijini nchini kunufaika kwa kujipatia kipato cha uhakika na maisha bora-Shahiri ikivunwa inasindikwa na kuwa kimea,malighafi ambao inatumika kutengenezea vinywaji vya bia-Shahiri inayozalishwa nchini inakidhi mahitaji ya viwanda 2 vya TBL Group vilivyopo katika mikoa ya Arusha na Mwanza ,kwa viwanda vingine inaagiza malighafi hiyo kutoka nje ya nchi.Kwa upande wa kilimo cha zabibu,TDL kampuni tanzu ya TBL Group inaendelea kuwezesha wakulima wa zao la zabibu mkoani Dodoma kupitia mpango wa kilimo shirikishi na hadi sasa wakulima zaidi ya 700  kutoka vijiji vya     Bihawana, Mpunguzi,, Mvumi, Hombolo, Mbabala, Veyula, Makang’wa, Mzakwe  na Mbalawala wamenufaika na mpango huu .

Wakulima wadogo wadogo wa zabibu kupitia mpango huu wanawezeshwa kupatiwa mafunzo ya kilimo yanayotolewa kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti wa kilimo ya Makutupora Viticulture Training and Research Center (MVTRC),pia kupitia mfuko ujulikanao kama Konyagi Social Trust - Zabibu na Shule Kwanza watoto wa wakulima waliopo kwenye mpango huu wanawezeshwa kulipiwa gharama za kupata elimu ya msingi na sekondari  hususani watoto wa kike ambao wamekuwa wakiachwa nyuma katika jamii .

Mbali na kuongeza wigo wa ajira kupitia sekta ya kilimo,kampuni ya TBL Group inaongoza kwa kulipa kodi nchini ikiwa imechangia pato la serikali katika  kipindi cha miaka 10 kwa kiasi cha shilingi trilioni 2.3/-“Kampuni yetu imechangia kuleta maendeleo ya nchi ya Tanzania kwa njia ya kukusanya na kulipa kodi za serikali na imekuwa ikitunukiwa tuzo kutoka taasisi mbalimbali mojawapo ikiwa tuzo ya mlipa kodi bora kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA baada ya kuongoza kwa kukusanya na  kulipa kodi nchini katika kipindi cha miaka  4 mfululizo”.Alisema Jarrin.

Aliongeza kuwa kampuni ya TBL Group ambayo  ni mfano wa ubinafsishaji ulioleta mafanikio nchini  inawekeza  zaidi ya shilingi bilioni 150/-kwa ajili ya kuendeleza viwanda vyake ili viendane na teknolojia zenye viwango vya kimataifa sambamba na viwanda vilivyopo katika nchi zilizoendelea.

Jarrin alisema kampuni inavyo viwanda 10 vilivyopo katika mikoa mbalimbali nchini viwanda vyake vilivyopo  katika mikoa ya Dar es Salaam,Mwanza na Arusha  ni miongoni mwa  viwanda bora vya kampuni mama ya SABMiller vilivyopo katika nchi mbalimbali duniani.Viwanda vya TBL Mwanza na Mbeya ni  miongoni mwa viwanda vinavyoshikilia rekodi ya kuwa viwanda bora vya bia kwa nafasi ya juu ya 10 na 15 duniani.

Alisema bia zinazozalishwa na viwanda vya TBL Group zinatawala soko kwa asilimia 78%  baadhi yake zikiwa ni Safari, Kilimanjaro, Ndovu, Castle Lager na Castle Lite .Kampuni pia imekuwa kinara wa kutengeneza vinywaji vikali na mvinyo ambavyo navyo vinatamba katika soko kwa asilimia 73% baadhi yake vikiwa ni   - Konyagi, Valeur na Dodoma Wine - Pia kampuni inatengeneza pombe za asili baadhi yake zikiwa ni aina ya   – Chibuku and Nzagamba –ambazo zinatamba katika soko la vinywaji vya asili kwa asilimia  8% .Utafiti uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya utafiti wa matumizi ya bidhaa kwa walaji ya CanBack umebainisha kuwa matumizi ya pombe za asili unatawala soko la  vinywaji vyenye kilevi Tanzania kwa asilimia 50%

 Jarrin Alisema kutokana na ripoti ya utafiti huo wa kitaalamu,TBL Group imeboresha zaidi vinywaji vya asili aina ya Chibuku na Nzagamba vinavyotengenezwa na viwanda vyake vya DarBrew ambapo vinapatikana kwenye chupa za ukubwa wa aina mbalimbali kuwawezesha wateja kuvipata katika mazingira ya usafi wakati huohuo kulingana na uwezo wa vipato vyao.Kupitia vinywaji hivi kampuni imeanzisha mpango unaojulikana kama ‘Chibuku Mamas’ wa kuwawezesha wanawake  kuviuza na kujipatia mapato ambapo mpaka kufikia sasa umenufaisha wanawake zaidi ya 130 na wengine wanaendelea kujiunga.

Kuhusu mtazamo wake wa biashara za vinywaji katika siku za usoni,Mkurugenzi huyo wa TBL Group alisema zipo changamoto mbalimbali baadhi yake  wananchi wengi kutokuwa na vipato vikubwa vya kuwawezesha kumudu kununua bia ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya watanzania wana vipato visivyozidi shilingi 5,000/-kwa siku,changamoto nyingine aliibainisha kuwa ni kutorasimishwa kwa pombe za asili ambazo zinashindana na vinywaji vilivyorasimishwa kwenye soko pia kutokuwepo  motisha za kuzalisha malighafi za kutengeneza vinywaji kama vile kupatikana Shahiri ya kutosha.

Akitoa maoni yake kuhusu namna ya kuendeleza sekta hii ili iweze kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa alisema ni kupunguza kodi mbalimbali kwenye vinywaji ikiwemo kupunguza kodi kwenye malighafi zinazozalishwa nchini kama kwenye kimea malighafi inayotumika kutengenezea bia inayozalishwa nchini ikiwemo kurasimisha pombe za asili  “Pamoja na changamoto hizi na nyinginezo kampuni inaendeleza mkakati wa kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano kuifanya Tanzania nchi ya viwanda na tayari tumethibitisha kuwa dhana hii inatekelezeka kwa kuwa na viwanda bora hapa vinavyotambulika kimataifa”.Alisema Jarrin.
Posted by MROKI On Sunday, August 21, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo