Nafasi Ya Matangazo

July 25, 2016

Rais John Magufuli akisalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein katika Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwenye uwanja wa Mashujaa, Julai 25, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Rais John Magufuli akisalimiana na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi,Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein katika Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwenye uwanja wa Mashujaa, Julai 25, 2016.  Kulia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubei Ali Maulid na wapili kulia ni Spika wa Bunge, Dkt, Tulia Ackson. 
Wananchi wa Dodoma waliojitokeza kushiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwenye uwanja wa Mashujaa mjini Dodoma leo.
***********
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi watanzania kuwaenzi Mashujaa kwa kudumisha Amani, Umoja na Utulivu uliojengwa na mashujaa hao.

Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mjini Dodoma.

Pamoja na kutoa rai hiyo Rais Magufuli ameahidi kuwa atahakikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma inatekelezwa kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano.

"Tunapoadhimisha siku ya Mashujaa hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa alisema makao makuu yawe Dodoma, haiwezekani sisi watoto wake, sisi wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.

"Kwa hiyo nilikwishazungumza na leo narudia hili katika siku ya Mashujaa, mlinichagua ndugu zangu wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi minane imepita, nimebakiza miaka minne na miezi minne, nataka kuwathibitishia kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki nitahakikisha serikali yangu pamoja na mimi tunahamia Dodoma bila kukosa" Amesema Rais Magufuli.

Kufuatia maelekezo hayo ya Mhe. Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza Mawaziri wote waanze mara moja kuhamia Dodoma na kwamba yeye mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mabalozi na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa vyama vya siasa na dini, maafisa na askari waliopigana vita mbalimbali.
Posted by MROKI On Monday, July 25, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo