Nafasi Ya Matangazo

June 28, 2016

KUMEKUWEPO na taarifa mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zinazotokana na habari iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo la tarehe 24 Juni, 2016, toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari "Sasa ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba".

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI HAUTAPIMWA NYUMBA KWA NYUMBA bali itafanya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania kuanzia mwezi Septemba 2016 ambapo UKIMWI utapimwa kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine nyingi ambazo hazitahusika moja kwa moja katika utafiti huu.

Utafiti huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na utahusisha watu wazima wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.  BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
Aidha, katika utafiti huu kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia dawa hizo. 

Ifahamike kwamba, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016 unafanyika nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003, wa pili ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011. 

Hivyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa utafiti huu sio mpya katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90.

Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utaendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).

Posted by MROKI On Tuesday, June 28, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo