Nafasi Ya Matangazo

June 03, 2016

Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Njombe Richard Moshi(kulia) akimshukuru Kiongozi wa Timu ya Uzinduzi Dkt Peter Kilima mara baada kufunga mafunzo ya uzinduzi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma kwa Halmashauri za Mkoa wa Njombe.
Kiongozi wa timu ya Uzinduzi Dkt.Peter Kilima akisisitiza jambo wakati wa mafunzo ya Uimarishaji Mifumo ya Sekta za umma mkoani Njombe.
Mkurugenzi Msaidizi, Uismamizi Rasilimali watu Ofisi ya Rais TAMISEMI Miriam Mmbaga akitoa nasaha mara baada ya kufungwa kwa uzinduzi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma mjini Njombe.
Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe Assumpter Mshama akizungumza kwenye kikao kilichozishirikisha Halmashauri 6 za Mkoa wa Njombe
************
HALMASHAURI 2 za Makete na Wanging’ombe mkoani Njombe zimechaguliwa kuingia katika awamu ya kwanza ya  mafunzo ya Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).

Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na Shirika la Msaada la Kimataifa la Marekani USAID yatawahusisha Wenyeviti wa Halmashauri,Wakurugenzi pamoja na wakuu wa Wilaya.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa Halmashauri hizo Kiongozi wa timu ya Uzinduzi Dkt Peter Kilima alisema Halmashauri hizo zimechaguliwa kuwa za mwanzo kushiriki mafunzo hayo kutokana na changamoto walizonazo.

‘’Vigezo vya uhitaji vimewapa nafasi ya kwanza kushiriki mafunzo haya kwa Madiwani ingawa halmashauri zote za Mkoa wa Njombe zitapata mafunzo hayo kwa awamu ya pili’’
Alisema mafunzo hayo yanatarajia kuanza Jumatatu ijayo mjini Njombe na kutolewa na wataalamu wa mafunzo kutokea mjini Dodoma.

Akizungumzia kuteuliwa kwa Halmashauri ya Makete,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Egnato Mtawa alisema anaamini changamoto zilizopo zimetoa kipaumbele kwao kuwa wa mwanzo kupata mafunzo hayo.

‘’Changamoto za Wilaya yetu zimetupa kipaumbele kuteuliwa wa mwanzo kupata mafunzo kwa Madiwani,tuna changamoto za jiografia na Miundo mbinu, tunaamini hatimaye changamoto tulizonazo zitapatiwa ufumbuzi’’ alisema Mtawa.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe Assumpter Mshama alisema mafunzo hayo kwa Madiwani yataongeza weledi wa utendaji kazi kwa watumishi  kutokana na Halmashauri hiyo kuwa mpya.

Awali akizungumza mara baada ya kufungwa kwa uzinduzi huo Mkurugenzi Msaidizi, Usimamizi wa Rasilimali watu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Miriam Mmbaga alisema kukosekana kwa maadili kwa watumishi wa umma ndiko kunakosababisha Halmashauri nyingi zipate hati zenye mashaka.

Alifafanua kuwa maadili yanayoelezwa ni yale yale yaliyopo katika imani za dini kwa kuwa vitabu vya dini zote zinapinga vitendo viovu ikiwemo rushwa.

‘’Dini zote zinapinga rushwa, maadili ya utumishi wa umma ni yale yale yaliyopo kwenye vitabu vya Uislamu na Ukristo,’’ alisisitiza.
Posted by MROKI On Friday, June 03, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo