Nafasi Ya Matangazo

June 24, 2016

NAIBU katibu mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Emmanuel Kalobelo (pichani juu) amewahimiza wafanyakazi wa shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es salaam (DAWASCO), kutekeleza na kufuata kanuni bora za maadili ya utendaji wa kazi zilizowekwa kwa watumishi wa umma ili kutoa huduma bora kwa wateja na  umma wote.

Akizungumza na wafanyakazi wa DAWASCO, katika kikao cha pamoja cha kuhitimisha  maadhimisho ya wiki ya utumishi kwa umma, naibu Katibu Mkuu amewataka wafanyakazi wote kuhakikisha kuwa wanazifahamu na kuzishika kanuni za  utumishi wa umma zilizowekwa na serikali ikiwamo kanuni ya kutoa huduma bora kwa wateja, kutoa huduma bila upendeleo pamoja na kuweka bidii katika kazi na kuwajibika kwa umma.

“Sisi tuko hapa kama watumishi wa umma, sote tunawajibika katika kuwapatia wananchi huduma ya Majisafi na salama, hivyo fanyeni kazi kwa umoja na kujituma ili kuwapatia wananchi huduma bora” alisema Mhandisi Kalobelo
Alifafanua kuwa wizara imepokea agizo la serikali la kuitaka kila wizara pamoja na taasisi kuadhimisha wiki ya utumishi kwa umma kwa kutenga siku maalum ya kusikiliza na kupokea na kuzifanyia kazi kero za  wateja wake. 

“Ninyi ni sehemu ya wateja wetu, sote tuko kwenye sekta ya Maji, tuko hapa kusikiliza pamoja na kujadili kero zinazokwamisha utoaji wa huduma bora ya Maji kwa wateja wenu kwani mkifanya vizuri DAWASCO kumbe inaonesha kuwa wizara imefanya vizuri pia” alisema Mhandisi Kalobelo.

Aidha, Naibu katibu Mkuu huyo aliweza kufanya mazungumzo na baadhi ya wateja kutoka kituo cha Dawasco Magomeni alipotembelea kituoni hapo, ambapo wateja wengi wameonyesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa, na wamepongeza juhudi zinazofanywa na uongozi wa kituo hicho za kuwapatia huduma ya Majisafi, wamemuiomba wizara kuwafanyia kazi wale wote ambao wanaonekana kulihujumu shirika (vishoka).

“Kwa kweli huduma tunayopata hapa magomeni kwa sasa ni nzuri, siwezi kabisa kusema tofauti, wamejitahidi sana kuboresha huduma ya Maji, tunaomba naibu katibu mkuu pamoja na wizara yako mtusaidie kuwaondoa hawa vishoka kwani wanasababisha wananchi wengine mtaani kukosa Maji alisema Bw. Mohamed Mponda.

Wiki ya Utumishi wa Umma ni moja ya tukio muhimu katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU) ambayo huadhimishwa kutambua mchango wa watumishi wa umma barani Afrika katika kuleta maendeleo ikiwamo kutatua changamoto zinazowakabili katika kutekeleza majukumu. Wiki hii huadhimishwa na nchi wanachama wa umoja wa Afrika kwa wakati mmoja.
Posted by MROKI On Friday, June 24, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo