Nafasi Ya Matangazo

May 10, 2016

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga

SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imetangaza rasmi tozo zitakazotumika katika Daraja la Nyerere jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga, amesema kuwa tozo hizo zitaanza kutumika rasmi Jumamosi wiki hii na zitahusisha vyombo vyote vya usafiri.

“Hakikisheni mnazifahamu tozo zote zitazotumika katika daraja hili kwa magari ya aina zote ili kuondoa usumbufu wakati wa utekelezaji wa zoezi la malipo”, Amesema Eng. Nyamhanga.
Katibu Mkuu huyo amezitaja tozo hizo kuwa ni pikipiki zitatozwa shilingi 600, mikoteteni, Guta, Bajaji, na magari madogo yatatozwa shilingi 1500, wakati magari aina ya ‘pick up’ yatakayozidi tani mbili na mashangingi yatatozwa shilingi 2000.

Amefafanua kuwa mabasi yanayobeba abiria wasiozidi 15(mini bus) yatatozwa shilingi 3000, mabasi yanayobeba abiria kuanzia 15 hadi 29 yatatozwa shilingi 5000. Mabasi yanayobeba abiria zaidi ya 29, Trekta na magari makubwa yenye uzito wa tani 2-7 yatatozwa shilingi 7000.

Ameongeza kuwa matrekta yenye matrela, magari makubwa yenye uzito wa tani saba hadi 15 yatatozwa shilingi 10,000 wakati magari yenye uzito wa tani 15 hadi 20 yatatozwa shilingi 15,000.

Katibu Mkuu Nyamhanga ameongeza kuwa magari yenye uzito usio wa kawaida (abnormal load) yatapita kwa vibali maalum vinavyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na kusisitiza kuwa tozo zote zimezingatia maoni ya wadau na hali ya uchumi wa wananchi ili kumudu gharama za matumizi ya daraja hilo.

“Magari yote ya Serikali na taasisi za umma yatatakiwa kulipa tozo kama ilivyobainishwa isipokuwa yale yenye namba za jeshi (Magereza, Polisi, JWTZ, Zimamoto) na magari ya wagonjwa”, amesisitiza Eng. Nyamhanga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (N.S.S.F), Yacoub Kidula, amewataka wananchi kuchangia gharama za uendeshaji wa daraja hilo ili kuongeza mapato ya Serikali.

Takribani wiki tatu magari yamekuwa yakivuka katika Daraja la Nyerere bila tozo ambalo lilifunguliwa katikati ya mwezi Aprili mwaka huu na Rais wa awamu ya Tano Mhe. John Pombe Magufuli.
Posted by MROKI On Tuesday, May 10, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo