Nafasi Ya Matangazo

May 08, 2016


MWENYEKITI wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi kesho Mei 9, 2016 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kuiga timu ya soka ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kama jina la Serengeti Boys inayotarajiwa kwenda India Jumatano Mei 11, mwaka huu.

Hafla ya kuiga timu hiyo, itayokahudhuriwa pia na Balozi wa India nchini, Mheshimiwa Sandeep Arya, inatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ulioko kwenye makutano ya barabara za Uhuru na Shaurimoyo, Ilala jijini Dar es Salaam.
  
Katika hafla hiyo mbali ya kutoa nasaha, Dioniz Malinzi ataikabidhi bendera timu ya Serengeti Boys inayokwenda Goa, India kushiriki mashindano maalumu ya soka ya kimataifa kwa vijana (AIFF Youth Cup 2016 U-16) yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIFF).

Mbali ya washiriki wenyeji ambao ni India, pia michuano hiyo itayoanza Alhamisi Mei 12, 2016, itashirikisha timu timu za taifa za vijana kutoka nchi za Marekani, Korea Kusini, Malaysia na Tanzania ambapo michezo itachezwa kwa mfumo wa ligi kwa kila timu kucheza michezo minne.

AIFF kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.

Tayari Serengeti Boys imescheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa mpaka sasa, mmoja dhidi ya Burundi na miwili dhidi ya timu ya vijana wa Misri (The Pharaohs) na kupata matokeo mazuri na tangu Aprili, 2016 iliweka kambi katika hosteli za TFF zilizopo Karume kujiandaa kwa safari chini ya Kocha Bakari Shime, akisaidiwa na Sebastian Mkomwa chini ya mshauri wa ufundi wa timu za vijana Kim Poulsen.

Ratiba ya michuano inaonyesha kwamba Tanzania itafungua dimba na Marekani kwenye Uwanja wa Tilak Maidan, Vasco, Goa huku mchezo wa pili ukiwa kati ya wenyeji India dhidi ya Malysia Mei 15, mwaka huu.

Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 17, kucheza na wenyeji India mchezo wa kwanza, Mei 19 Serengeti Boys watacheza dhidi ya Korea Kusini na mchezo wa mwisho watamaliza dhidi ya Malysia Mei 21.

Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25 ambapo kabla ya mchezo wa fainali, utchezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa.


Kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo maalumu ya vijana kimataifa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Serengeti Boys, kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za vijana barani Afrika dhidi ya Shelisheli Juni 25 hadi Julai 2, 2016.
Posted by MROKI On Sunday, May 08, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo