Nafasi Ya Matangazo

April 01, 2015



Sehemu ya wanachuo wa ADEM wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano Bw. Cosmas Mwaisobwa (haonekani kwenye picha hii).


********

Uelewa mdogo wa masuala ya utoaji wa mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu umeendelea kuwa chanzo cha baadhi ya wahitaji wa mikopo kulalamika bila kwanza kutafuta chanzo cha wao kutopata mikopo hiyo.

Hayo yamebainika hii leo katika ziara ya mafunzo ya wanachuo 147 kutoka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) unaoendeshea shughuli zake Bagamoyo mkoani Pwani waliofika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa ziara ya mafunzo.

Miongoni mwa maswali yaliyoulizwa na wanachuo hao ni pamoja na uwezekano wa wafanyakazi kupatiwa mikopo, vigezo vya utoaji mikopo na jinsi ya kubaini waombaji wa mikopo wenye sifa za kupata mikopo hiyo. Maswali mengine yalilenga kujua jinsi Bodi inavyowatambua wanufaika wa mikopo ambao mikopo yao imeiva tayari kurejeshwa.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano Bw. Cosmas Mwaisobwa aliwasilisha mada iliyojumuisha  historia fupi ya Bodi, Sera ya Uchangiaji, Muundo wa Uongozi, Utaratibu wa Utoaji Mikopo na Utaratibu wa Urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanachuo hao, Mkufunzi aliyeandamana  nao Bibi Rhoda Samwepa, ameelezea kufurahishwa kwake na jinsi Bw. Mwaisobwa ambaye pia ni Msemaji wa Bodi, alivyotolea ufafanuzi kwa ufasaha masuala yanayoonekana kuwa na utata kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kwamba anaona umuhimu wa wanufaika kurejesha mikopo hiyo ili wahitaji wengine waweze kunufaika.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikipokea makundi mbalimbali ya wadau wa elimu wanaofika kwa lengo la kujifunza masuala ya utoaji mikopo, vigezo na masharti ya utoaji mikopo na utaratibu wa kurejesha mikopo hiyo na hivyo kuendelea kuongeza uelewa wa mikopo ya wanafunzi kwa idadi kubwa zaidi ya wadau.
Posted by MROKI On Wednesday, April 01, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo