Nafasi Ya Matangazo

January 28, 2015

Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Othman Chande (Kulia) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari  kuhusu maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mwaka 2015. Maadhimisho hayo  yanaongozwa na maudhui yasemayo  “ Fursa ya kupata haki: wajibu wa Serikali, Mahakama na wadau”. Kushoto ni Mh. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama.
 ***********
 Rais Jakaya Kikwete anatarijiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya sheria nchini (Law Day) itakayofanyika Februari 4, 2015, katika viwanja vya mahakama vilivyopo mtaa wa Chimala jijini Dar es salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania Mh. Othman Chande amesema kuwa maadhimisho hayo kwa mwaka huu yanaongozwa na maudhui yasemayo  “ Fursa ya kupata haki: wajibu wa Serikali, Mahakama na wadau”.


 Amesema kwa mara ya kwanza maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya Wiki ya   Shera yatakayofanyika  katika viwanja vya Mnazi Mmoja   kuanzia  tarehe  30 Januari  2015  hadi  tarehe  2 Februari  2015 .


Mh.Chande ameeleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na maonesho ya Wiki ya Sheria yanaashiria mwanzo wa shughuli za mahakama kwa mwaka 2015  na kufafanua kuwa kipaumbele kitatolewa katika kupunguza mrundikano wa mashauri ya muda mrefu yaliyoko mahakamani na kushughulikia mashauri yenye mvuto mkubwa kijamii,miradi mikubwa, uhujumu uchumi, madawa ya kulevya, Biashara ndani na nje ya nchi na Rushwa.


Kuhusu maonesho hayo amesema yanalenga  kutoa elimu kwa wadau wa sheria na huduma za kisheria kwa wananchi kuhusu Ufunguaji na uendeshaji wa mashauri mbalimbali hasa mirathi, Utatuzi wa migogoro kwa njia ya suluhu, kueleza mfumo mpya wa ulipaji wa tozo za kimahakama kwa njia ya benki, Kutoa msaada wa kisheria, kutolewa vyeti vya mawakili, kupokea maoni na malalamiko kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.


Ameeleza kuwa wadau wakuu  watakaoshiriki katika maonesho hayo ni Mahakama, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto, Taasisi ya Mafunzo ya Uansheria kwa vitendo Tanzania na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.


Wadau wengine ni Taasisi zinazotoa msaada wa kisheria, TAKUKURU, Jeshi la Polisi, Magereza, Chama cha Mawakili Tanganyika na Tume ya kurekebisha sheria.


Amesema pamoja na maonesho hayo kutakuwa na matembezi maalum ya kuadhimisha Wiki ya Sheria tarehe 1 Februari 2015 yatakayoongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili Mh. Ali Hassan Mwinyi kuanzia Mahakama Kisutu kupitia barabara za Serena-Ohio, Gymkana –Obama Road, Mahakama ya Biashara, Barabara ya Kivukoni, Sokoine , Railway, Nkurumah, Lumumba na Mkunguni hadi Mnazi Mmoja.
Posted by MROKI On Wednesday, January 28, 2015 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo