Nafasi Ya Matangazo

January 21, 2013

Kwa wiki ya tatu mfululizo kumekuwa na malumbano kuhusiana na suala la ujenzi wa Bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Kumekuwa na madai yenye nguvu ya hoja kutoka kwa wananchi wa Mtwara dhidi ya porojo kutoka kwa viongozi wenye dhamana ya kujibu madai haya ya watu wa Mtwara. Watu wa Mtwara kwa umoja wao na kwa kuungwa mkono na viongozi wa dini zote wamekuwa wakitaka Serikali ifikirie upya suala la mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi na badala yake kujenga mitambo ya kufua umeme mkoani Mtwara na kusafirisha umeme huo kwenda maeneo mengine ya nchi. Kwenye moja ya maandishi yangu (Serikali iwasikilize watu wa Mtwara) nimeshauri kuwa Taifa liwe na gridi nyingine ya Taifa ambayo itatokana na Gesi tu na ianzie Mtwara.
Ikumbukwe kwamba katiba ya nchi, ibara ya 9 katika mabano J inataka mamlaka ya dola na vyombo vyake vyote kuhakikisha ya kwamba shughuli zote za kiuchumi zinaendeshwa kwa namna ya kwamba pasiwe mrundikano wa utajiri au shughuli za uzalishaji kwa watu wa chache. Katiba inaendela kwa kuelekeza kwamba uchumi wa nchi upangwe katika uwiano sawia (9, d). Watu wa Mtwara wanatekeleza matakwa haya ya katiba kwa kukataa mrundikano wa shughuli za kiuchumi wa nchi na utajiri wa nchi kua kwenye mikoa michache na hasa mkoa wa Dar-Es-Saalam.
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya porojo na kuwatusi watu wa Mtwara na kama ilivyozoeleka Rais Jakaya Kikwete na Mawaziri wake wamekuwa wakisema suala la Mtwara linatumika na wanasiasa kujitafutia umaarufu. Inasikitisha sana kuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwaambia mabalozi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini kuwa yanayoendelea mkoani Mtwara yanachochewa na Wanasiasa tuliosimama na wananchi wanaodai haki ya kufaidi utajiri wa nchi yetu. Rais Kikwete na Mawaziri wake wameshindwa kabisa kuonyesha uongozi katika suala hili na hatimaye kuhatarisha umoja wa kitaifa.
Kwa udhaifu wa serikali na tabia ya kutafuta mchawi badala ya kutatua tatizo la msingi, wananchi wameendelea kukutana na hata wengine sasa kuanza kusambaza ujumbe wa kukata kipande cha nchi na kuanzisha Jamhuri ya Kusini. Nimeona kwenye mabango ya mkutano wa hadhara uliofanyika 19/1/2013 wananchi wakibeba mabango yanayoaishiria kuchoka kuwa sehemu ya Tanzania na kuanzisha Jamhuri ya Makonde kuanzia jiwe la Mzungu wilayani Kilwa mpaka mto Ruvuma. Haya yanatoka na kiburi cha Serikali kujishusha na kuwasikiliza wananchi wanao dai haki yao ya kikatiba.
Ni Serikali iliyokosa uhalali wa kutawala inayoweza kudharau hisia hizi za wananchi. Serikali ielewe kwamba kamwe haitaweza kulinda kila nchi ya bomba hili iwapo italijenga kwa nguvu. Badala ya kuzungumza na vyombo vya habari Serikali ifanye mazungumzo na wananchi wa Mtwara na kukubaliana na matakwa yao. Kitendo cha Serikali kung’ang’ania msimamo wake dhidi ya watu wa mtwara ni kitendo kinacho weza kuipasua nchi na hivyo kwenda kinyume na masharti ya katiba ibara ya 28 ambayo inasema: “kila raia ana wajibu wa kulinda uhuru wa nchi, uhuru mamlaka na umoja wa taifa.”ibara ya 28, 1.
Inawezekana Serikali inaogopa kuvunja makubaliano na Wachina ya mkopo wa dola za kimarekani 1.2 bilioni ambao imeuingia bila hata kushirikisha Bunge. Inawezekana Serikali na hasa watendaji wa Serikali waliojadili mkopo huu wameshapata chao na hivyo kuogopa kusikiliza madai halali ya wananchi. Lakini yote hayo hayawezi kuwa zaidi ya Umoja wa nchi yetu. Hatuwezi kukubali nchi yetu ipasuke vipande vipande kwa sababu tu ya kulinda mkataba wa bilioni 1.2 tuliokopa China, ambayo serikali inang’ang’ania.
Tunafahamu kwamba ubalozi wa China umeandika barua serikalini kuwaondoa raia wa China waliopo Mtwara kwa hofu ya maisha yao. Serikali inaficha ukweli huu kama ilivyoficha ukweli kwamba Naibu Waziri wa Nishati na Madini bwana George Simbachawene alifukuzwa na wananchi wa Mtwara alipokwenda hivi majuzi. Serikali itaficha ukweli mpaka lini? Lazima tupate majawabu.
Kwanza Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa Bomba hili. Kamati ya Bunge ya POAC ilipokuwa inapitia mahesabu ya TPDC iliomba mkataba na kwa mshangao mkubwa wabunge wakaambiwa Mkataba haupo TPDC bali upo Wizarani. Kwa nini Mkataba huu wa matrilioni ya Fedha unafichwa? Mkataba huu ulisainiwa pamoja mikataba mingine 2, mmoja wa kujenga nyumba za wanajeshi wa thamani ya dola za kimarekani 400 milioni na mwingine wa mawasiliano jeshini wa dola za kimarekani 110 milioni, na mikataba yote mitatu imesainiwa kimya kimya bila kushirikisha wananchi kupitia Bunge. Lazima mikataba yote hii iwekwe wazi.
Pili, Mkataba huu uchunguzwe kama unalingana na thamani ya fedha maana kwa utafiti wa awali inaonyesha kuwa bei ya ujenzi wa bomba imepandishwa maradufu. Wastan wa kujenga bomba la gesi duniani ni dola za kimarekani 1.2 milioni kwa maili moja. Mradi huu wa Tanzania utagharimu dola za kimarekani 2.2 milioni kwa kilomita moja (maili 1 ni sawa na kilomita 1.6).
Tatu, Serikali ibadilishe Mkataba huu kuwa wa mkopo wa kujenga Mitambo ya kufua umeme Mtwara na ujenzi wa Msongo wa Umeme kama gridi ya pili ya Taifa. Kwa sasa Tanzania ina gridi moja ambayo inabebwa na bwawa la Mtera linalo tegemea mto Ruaha ambao hivi sasa unakauka miezi 5 katika miezi 12 ya mwaka. Ni dhahiri kwamba kwa usalama wa Taifa na hata kwa gharama Nchi itafaidika zaidi kwa kujenga gridi nyingine kutokea Mtwara badala ya kusafirisha gesi kuja Dar-Es-Salaam.
Serikali haitashinda vita hii kwa kuzusha kwamba ama wanasiasa wanaopinga wanatumika na makampuni mengine au kwa mataifa ya magharibi kutaka kuvuruga nchi. Serikali ijitazame yenyewe. Bila kufanya hayo tunayo pendekeza hapo juu, wananchi wataendelea kupigania hako yao. Hii ni vita ya uwajibikaji. Wananchi wanataka kufaidika na rasilimali za nchi yao. Kwa vyovyote vile upande wa wananchi utashinda. Vita ya uwajibikaji kwenye rasilimali za nchi sio ya vyama vya siasa, ni vita ya wananchi. Chama cha siasa kitakachokwenda kinyume na matakwa ya wananchi, kinajichimbia kaburi.
--
Zitto Kabwe

Posted by MROKI On Monday, January 21, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo