Nafasi Ya Matangazo

December 14, 2012

 Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Kituo cha Tanga, Dk. Mercy Chiduo akiwasilisha utafiti uliofannywa na kikundi cha watafiti wa NIMR nchini, juu ya uwezo wa dawa ya Ciprofloxacin kutibu ugonjwa wa Kisonono. Taarifa hiyo ya utafiti huo wa awali ilitolewa mbele ya Waandishi wa habari na Watafiti mbalimbali jijini Dar es Salaam leo Desemba 2012. 
**********
Na Mroki Mroki, FK Blog
UGONJWA wa zinaa wa Kisonono umekuwa sugu kutibika kwa kutumia dawa ya Ciprofloxacin na kusababisha wagonjwa kutokukopona.

Kutokufanya kazi kwa dawa hiyo kutibu ugonjwa wa Kisonono kumegunduliwa na kundi la watafiti wa Kitanzania kutoka Taaisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Kuongozwa na Mr. John Changalucha, wa NIMR Mwanza na kufanya utafiti juu ya ufanyaji kazi wa dawa hiyo kwa kutibu kisonono katika wilaya za Tanga, Moshi mjini, Dar es Salaam.

Akiwasilisha taarifa ya awali ya utafiti huo uliofanyika kuanzia Oktoba mwaka 2011 na kumalizika Aprili mwaka huu kwa hizo tatu kabla ya watafiti hao kumalizia Wilaya ya Mbeya Mjini, Dk. Mercy Chiduo kwa niaba ya Watafiti wenzake amesema Wilaya ya Moshi mjini ndio tatizo limebainika kuwa kubwa zaidi.

Dk. Mercy ameeleza kuwa Wilayani Moshi wagonjwa wote waliofanyiwa utafiti walionesha kutokupona kwa dawa hiyo ya Ciprofloxacin sawa na asilimia 100, huku Wilaya ya Tanga ulikuwa kwa asilimia 25 na Dar es Salaam ikiwa ni kwa asilimia 71.4.

Aidha mtafiti huyo anasema uwezo wa dawa hiyo kutibu Kisonono kwa utafiti huo ni sawa na asilimia 40 hivyo kuwa kinyume na sheria ya Shirika la Afya Duniani ambalo linagiza kuwa dawa ili iwepo katika orodha ya kutibu magonjwa husika ni lazima iwe na uwezo wa kutibu kwa asilimia 95.

Watafiti hao wamependekeza dawa za ceftriaxone, cefixime, azithromycin na spectinomycin zitumike kwa sasa kutibu ugonjwa wa Kisonono huku Ciprofloxacin ikibaki kutibu magonjwa mengine isipokuwa Kisonono.

Wagonjwa wapatao 353 walijitokeza katika utafiti huo katika vitengo vya Magonjwa ya Zinaa kwenye vituo vya afya vya Ngamiani jijini Tanga, Majengo mjini Moshi, na Zahanati ya IDC Jijini Dar es Salaam.

Kushindwa kwa dawa hiyo kutibu kunatokana na ugonjwa huo kuwa sugu kufuatia tabia ya wagonjwa wengi kujinunulia dawa bila kupatiwa vipimo vya daktari na hili linadaiwa kutokana na kuwepo kwa maduka ya dawa ambayo huwauzia wagonjwa dawa bila kuwa na vyeti vya daktari.

Utafiti huo wa uwezo wa dawa hiyo kutokutibu unakaribia kuendana na ule uliowahi kufanyika katika nchi za Israel (61%), Urusi (68%) Kanda ya Magharibi ya WHO (62%-70%), Afrika Kusini (42%), Japan (24.4%) na China (34.3%), huku Jiji la Mwanza-Tanzania, likionesha dawa hiyo kutokufanya kazi kwa asilimia 71 katika utafiti uliofanyika mapema.  
Posted by MROKI On Friday, December 14, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo