Nafasi Ya Matangazo

October 02, 2012


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza akitoa hotuba yake katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya iliyopo mjini Kibaha.
Mkurugenzi wa NHIF, Emanuel Humba akitoa maelezo ya utangulizi ya Mfuko kwa wageni walioalikwa katika hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Dk. Mpemba akitoa shukrani kwa Mfuko kwa ushirikiano wake katika uboreshaji wa huduma za matibabu katika hospitali ya Tumbi.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Mfuko na wageni waalikwa wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa.
Wakibadilishana mawazo ya uboreshaji wa huduma za matibabu mkoani Pwani.
Baadhi ya Wakurugenzi wa NHIF wakibadilisha mawazo kabla ya kuanza kwa hafla ya uzinduzi wa ofisi mpya.  

 Na Mwandishi Wetu 
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Bi. Mwantumu Mahiza ameutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuisaidia kwa hali na mali Hospitali ya Tumbi kutokana na umuhimu wake katika kuhudumia wagonjwa mbalimbali wakiwemo majeruhi wengi wa ajali zinazotokea katika maeneo ya mkoa huo. 

 Alisema kuwa kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili Hospitali hiyo ikiwemo ya kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa kwa siku, ukosefu wa Vifaa vya kisasa vya uchunguzi, kuna haja kubwa kwa NHIF kuingilia kati ili kuinusuru hospitali hiyo na maisha ya Watanzania kwa ujumla. 

 Bi. Mahiza aliyasema hayo jana katika uzinduzi wa Ofisi mpya ya NHIF iliyopo mkoani Pwani ambayo iliwakilisha Ofisi zingine mpya nane zilizopo katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Ruvuma, Rukwa, Singida, Lindi, Shinyanga, Kagera na Manyara ambazo zimefunguliwa na NHIF kwa lengo la kusogeza huduma kwa wanachama wake na kuboresha huduma kwa ujumla.

 “Nimefarijika sana kwa kutupa heshima kubwa Mkoa wa Pwani, mngeeamua kwenda Mkoa mwingine kuzindua ili kuziwakilisha ofisi zingine, Niwaombe sana wenzangu NHIF, mtupe umuhimu wa kipekee katika kutusaidia vifaa tiba na hasa kifaa cha kutunzia damu salama, inashangaza na haieleweki kwa wasomi kama sisi kuona ajali na wagonjwa wakiwa Pwani na damu ikitunzwa Dar es Salaam...nakuagiza Mganga Mkuu wasilisha ombi hilo NHIF haraka iwezekanavyo,” alisema Mahiza.

 Alisema kuwa suala la vifaa vya uchunguzi katika hospitali hiyo linamnyima usingizi kutokana na mazingira yanayoikabili hospitali hiyo ambayo kwa wastani inapokea wagonjwa 500 kwa siku. Akijibu ombi hilo la Mkuu wa Mkoa, Mjumbe wa Bodi ya NHIF, Bi. Mwanaidi Mtanda alisema kuwa Bodi itahakikisha inatoa kipaumbele katika suala hilo kwa lengo la kuwezesha hospitali hiyo kuwa na vifaa vya kisasa ili huduma bora kwa wanachama na wananchi kwa ujumla zipatikane.

 “Kwa niaba ya Bodi niseme kuwa Mfuko una nia ya dhati ya kusaidia Hospitali ya Tumbi na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kwa lengo la kuboresha huduma na pale tutakapopokea maombi kutoka kwenu yatafanyiwa kazi haraka sana,” alisema Bi. Mtanda. 

 Bi. Mtanda hakusita kusema kuwa hamasa ya utumiaji wa fursa inayotolewa na NHIF ya utoaji wa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa vituo hasa vya serikali bado ni mdogo hivyo akatumia fursa hiyo kuwaomba viongozi na wamiliki wa vituo vyote vya matibabu vilivyosajiliwa na Mfuko kuomba mikopo hiyo ili kuviwezesha vituo vyao kutoa huduma bora za matibabu. 

 Hata hivyo, Bi. Mwantumu alieleza wazi kuwa NHIF imekuwa chachu kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya kutokana na ukweli kwamba vituo vingi vinaendesha shughuli zake kwa kutumia fedha zinazolipwa na Mfuko huo. 

 “Mtu yeyote anayefuatilia mwenendo wa Sekta ya Afya nchini atakubaliana nami nikisema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, umekuwa chachu kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya kwani kwa kiwango kikubwa vituo vingi vinaendesha shughuli zake kwa fedha zinazolipwa na Mfuko huo hivyo nawapongeza na kuwataka muendelee kusaidia,” alisema. 

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa NHIF, Bw. Emanuel Humba alisema kuwa lengo la uzinduzi wa ofisi hizo ni kutaka kuwajulisha wadau kuwa Mfuko umesogeza huduma zake karibu na wanachama ikiwa ni njia mojawapo ya uboreshaji wa huduma. 

 Alisema pamoja na Mfuko huo kukua kwa kasi na kuwa na mafanikio makubwa lakini bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa dawa, vifaa tiba, upungufu wa wahudumu changamoto ambazo Mfuko unazifanyia kazi kupitia mipango mbalimbali ikiwemo ya kusajili maduka ya dawa muhimu na ukopeshaji wa vifaa tiba. NHIF kwa sasa ina mtandao wa ofisi zake katika Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar isipokuwa mikoa mipya.
Posted by MROKI On Tuesday, October 02, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo