Nafasi Ya Matangazo

April 14, 2012

Ndugu zangu,
KUNA wengi  tunaokumbuka tulikuwa wapi siku ile ya tarehe 12 Aprili, 1984 wakati Mwalimu Nyerere alipolitangazia taifa kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine kilichotokana na ajali ya gari eneo la Wami-Dakawa  akiwa njiani kutoka Dodoma kwenda Dar.

Kwa bahati mbaya, vijana wengi waliozaliwa baada ya 1984 hawajui sana habari za Edward Moringe Sokoine . Mimi nilikuwa Kidato cha Pili tu pale Sekondari ya Tambaza. Nakumbua ilikuwa majira ya saa kumi jioni.  Nilikuwa natembea kwa miguu kutoka Kinondoni ’ A’ kuelekea nyumbani Kinondoni Biafra. Nilipofika maeneo ya jirani na Msikiti wa Mtambani nikasikia wimbo wa taifa unapigwa.

Nilihisi haraka kuna jambo kubwa la kitaifa limetokea. Nikasogea kwenye duka la jirani. Wapita njia wengine nao walisogea mahali hapo. Wimbo wa Taifa ulipomalizika, nikamsikia Mwalimu akianza kutamka kwa sauti ya huzuni; ” Ndugu Wananchi, leo hii…” Kilichofuata ni historia ambayo hapa nashiriki kuiandika.

Naam, Sokoine alikuwa kiongozi wa kweli ambaye daima alisimama upande wa umma. Ni Sokoine aliyetufanya hata tuliokuwa sekondari  wakati huo, tuwe na imani na uongozi wa nchi. Tuwe na matumaini ya maisha bora kwa siku za baadae.

Ndio, ukitoka kwa Mwalimu, ni Sokoine pia aliyechangia katika kutufanya watoto wa wakati huo, tuamini na tuipende siasa. Alikuwa mfano wa kuigwa. Alishi kama alivyohubiri. Siyo tu hakujilimbikizia mali, halipunguza hata mali zake ili apate nafasi zaidi ya kututumikia Watanzania.
Itakumbukuwa, kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Aprili, 1984, Sokoine alikabiliana n ahoja za wabunge kutaka kuongezewa posho na marupurupu yao. Sokoine alitamka;

”  Ndugu Spika, niko tayari kuwaongezea wabunge posho ya chakula chao, lakini kamwe sitakuwa tayari kuwaongezea mishahara na marupurupu mengine.” Mwisho wa kunukuu. Huyo ndiye Edward Moringe Sokoine.  Alikuwa kiongozi wa kanuni na mwenye msimamo usioyumba.

Sokoine alielewa, kuwa ukiwalinganisha na wananchi walio wengi, wabunge walikuwa na hali bora zaidi kimaisha. Alikuwa tayari kuchukiwa na wabunge kwa kutetea maslahi ya wanyonge, kuliko kupendwa na wabunge kwa kujali zaidi maslahi yao. 

Baada ya kikao kile cha Bunge, Edward Sokoine, badala ya kupanda ndege ya Serikali kumrudisha Dar es Salaam, aliamua kurudi Dar Es Salaam kwa njia ya barabara, afanye hivyo ili mle anamopita apate nafasi ya kuona shughuli za maendeleo zifanywazo na wananchi. Sokoine hakufika Dar Es Salaam, mauti yakamchukua kwa ajali ya gari pale Wami- Dakawa, Morogoro.
Leo tuna viongozi wa wananchi wenye kutanguliza mbele maslahi yao binafsi. Viongozi wasiotosheka na posho ya elfu sabini ya kikao. Viongozi wenye kufikiria tu ’ kamuhogo kao’. Wanafikiri magari na marupurupu yao badala ya masuala yenye kuwahusu  wananchi wa kawaida.

Je, Sokoine angefufuka leo ingekuwaje?
Bila shaka angefufuka na kufa tena ndani ya siku saba. Maana, Sokoine angeshangaa kuwaona wabunge wa leo wakichukua posho  ya kikao cha siku moja sawa na mshahara wa miezi miwili au mitatu kwa Watanzania walio wengi. 

Sokoine angeshangaa kuona wabunge hawatembelei tena Landrover za bei nafuu bali magari ya kifahari huku wananchi walio wengi bado wanaishi kwenye nyumba za udongo na nyasi. Kwamba bado kuna wanyonge wengi wasio na hakika ya kula yao ya leo na kesho huku wananchi wakiambiwa, tena na Spika wa Bunge, kuwa Bunge ni eneo la umasikini!

 Sokoine angeshangaa kusikia kuwa uongozi siku hizi unanunuliwa, na hata yeye akijaribu tena kuingia Bungeni atalazimika agawe ’ Vimuhogo’ kwa watakaompitisha kwenye kura za maoni.  Sokoine angeshangazwa pia kusikia, kuwa kuna mawaziri na watendaji wakuu serikalini wanaokaa mahotelini kwa kukosa nyumba za serikali kwa vile umepitishwa uamuzi wa kuziuza, kisha kujenga nyingine na kuziuza tena! 

Lakini, Sokoine angeshangaa zaidi kuona Watanzania aliowaacha mwaka 1984 wamechelewa sana kuamka na kupambana kuibadili hali iliyopo. 

Naam, Sokoine angefufuka leo, angesononeka sana kuona pengo pana  lililopo kati ya wenye nacho na wasio nacho. Kati ya viongozi na wananchi. 

Edward Moringe Sokoine, Daima Tutakukumbuka.
Posted by MROKI On Saturday, April 14, 2012 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo